JUMAPILI YA 6 YA PASAKA

MADA YA JUMAPILI: Ahadi ya Roho Mtakatifu.

Cha msingi katika masomo ya leo ni ahadi yake Kristo kumtuma Msaidizi, Roho wa kweli. Ujio wa Roho itaadhimishwa katika sherehe ya Pentekoste. Injili ya leo inakidiri jinsi itupasavyo kujitayarisha kumpokea Roho huyu. Somo la 2 ladhihirisha utimilivu wa mafunzo haya kwa maisha ya Wakristo wanaostahimili mateso wakijua kwamba Msaidizi huyu daima yu pamoja nao. Somo la kwanza linadhihirisha jinsi mitume walivyomwita Roho kuja kwa maombi na kuwawekelea mikono.

SOMO LA 1: Matendo. 8:5-8, 14-17.

Filipo alitelemka akaingia mji wa Samaria, akawahubiri Kristo. Na makutano kwa nia moja wakasikiliza maneno yale yaliyosemwa na Filipo walipoyasikia na kuziona ishara alizokuwa akizifanya. Kwa maana pepo wachafu wakawatoka wengi waliopagawa nao, wakilia kwa sauti kuu; na watu wengi waliopooza, na viwete, wakaponywa. Ikawa furaha kubwa katika mji ule. Na mitume waliokuwako Yerusalemu, waliposikia ya kwamba Samaria imelikubali neno la

Mungu, wakawapelekea Petro na Yohana; ambao waliposhuka, wakawaombea wampokee Roho Mtakatifu; Kwa maana bado hajawashukia hata mmoja wao, ila wamebatizwa tu kwa jina lake Bwana Yesu. Ndipo wakaweka mikono yao juu yao, nao wakampokea Roho Mtakatifu.

NENO LA MUNGU.

Zaburi. 66:1-7, 16, 20, (K) 1.

(K). Mpigie Mungu kelele za shangwe, nchi yote,  au:  Aleluya!

Mpigie Mungu kelele za shangwe, nchi yote, Imbeni utukufu wa jina lake, Tukuzeni sifa zake. Mwambieni  Mungu, Matendo  yako yatisha kama nini! (K).

Nchi yote itakusujudia na kukuimbia, Naam, italiimbia jina lako. Njoni yatazameni matendo ya Mungu; Hutisha kwa mambo awatendayo wanadamu. (K).

Aligeuza bahari ikawa nchi kavu; Katika mto walivuka kwa miguu; Huko ndiko tulikomfurahia. Atawala kwa uweza  wake milele. (K).

Njoni, sikieni, ninyi nyote mnaomcha Mungu, Nami nitayatangaza aliyonitendea roho yangu. Na ahimidiwe Mungu  asiyeyakataa maombi yangu, Wala kuniondolea fadhili zake. (K).

SOMO LA 2: 1 Petro. 3:15-18.
Mwe tayari sikuzote kumjibu kila mtu awaulizaye habari za tumaini lililo
ndani yenu; lakini kwa upole na kwa hofu. Nanyi mwe na dhamiri njema, ili katika neno
lile mnalosingiziwa, watahayarishwe wale wautukanao mwenendo wenu mwema katika
Kristo. Maana ni afadhali kuteswa kwa kutenda mema, ikiwa ndiyo mapenzi ya Mungu,
kuliko kwa kutenda mabaya. Kwa maana Kristo naye aliteswa mara moja kwa ajili ya
dhambi, mwenye haki kwa ajili yao wasio haki, ili atulete kwa Mungu; mwili wake
akauawa, bali roho yake akahuishwa.
NENO LA MUNGU

SHANGILIO: Yohana. 14:23.
Aleluya. Yesu alisema: Mtu akinipenda, atalishika neno langu;
na Baba yangu atampenda; nasi tutakuja kwake.
Aleluya.

INJILI: Yohana. 14:15-21.
Yesu aliwaambia wafuasi wake: ‘Mkinipenda, mtazishika amri zangu. Nami nitamwomba
Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele; ndiye Roho wa kweli;
ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala haumtambui; bali
ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu. Sitawaacha ninyi
yatima; naja kwenu. Bado kitambo kidogo na ulimwengu haunioni tena; bali ninyi
mnaniona. Na kwa sababu mimi ni hai, ninyi nanyi mtakuwa hai. Siku ile ninyi mtatambua
ya kuwa mimi ni ndani ya Baba yangu, nanyi ndani yangu, nami ndani yenu. Yeye aliye
na amri zangu, na kuzishika, yeye ndiye anipendaye; naye anipendaye atapendwa na Baba
yangu, nami nitampenda na kujidhihirisha kwake.’
INJILI YA BWANA.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *