SHEREHE YA MWILI NA DAMU TAKATIFU YA BWANA WETU YESU KRISTU

Juni 14 2020

MWILI NA DAMU YA KRISTO
Mada ya Jumapili: Chukua Ule! Masomo yote tatu yanatusaidia kutafakari kuhusu maana ya Ekaristi. Somo la 1 yazungumzia manna, zawadi lisilotarajiwa kutoka kwa Mungu kwa Waizraeli jangwani, lililowapa uhai. Injili yazungumzia zawadi bora zaidi kuliko manna, mkate uletao uzima wa milele. Somo la 2 latufundisha kwamba Ekaristi, sio mkate wakuliwa kibinafsi, bali humegwa na kuliwa kwa pamoja kama ishara ya umoja.

SOMO LA 1: Kumbukumbu la Torati. 8:2-3; 14-16a.
Musa aliwaambia makutano: Nawe utaikumbuka njia ile yote Bwana, Mungu wako, aliyokuongoza miaka hii arobaini katika jangwa, ili akutweze, kukujaribu, kuyajua yaliyo moyoni mwako, kwamba utashika amri zake, au sivyo. Akakutweza, akakuacha uone njaa, akakulisha kwa mana, usiyoijua wewe wala baba zako hawakuijua; apate kukujulisha ya kuwa mwanadamu haishi kwa mkate tu, bali huishi kwa kila litokalo katika kinywa cha Bwana. Basi hapo moyo wako usiinuke, ukamsahau Bwana, Mungu wako, aliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa; aliyekuongoza katika jangwa lile kubwa lenye kitisho, lenye nyoka za moto na nge, nchi ya kiu isiyokuwa na maji; aliyekutolea maji katika mwamba mgumu, aliyekulisha jangwani kwa mana, wasiyoijua baba zako.
NENO LA MUNGU.

Zaburi. 147:12-15, 19-20. (K) 12.
(K). Msifu Bwana, Ee Yerusalemu.

Msifu Bwana, Ee Yerusalemu; Msifu Mungu wako, Ee Sayuni. Maana ameyakaza mapingo ya malango yako, Amewabariki wanao ndani yako. (K).
Ndiye afanyaye amani mipakani mwako, Akushibishiaye kwa unono wa ngano. Huipeleka amri yake juu ya nchi, Neno lake lapiga mbio sana. (K).
Humhubiri Yakobo neno lake, Na Israeli amri zake na hukumu zake. Hakulitendea taifa lo lote mambo kama hayo, Wala hukumu zake hawakuzijua. Aleluya. (K).

SOMO LA 2. 1 Wakoritho 10:16-17.
Kikombe kile cha baraka tukibarikicho, ‘Je! si ushirika wa damu ya Kristo? Mkate ule tuumegao, si ushirika wa mwili wa Kristo? Kwa kuwa mkate ni mmoja, sisi tulio wengi tu mwili mmoja; kwa maana sisi sote twapokea sehemu ya ule mkate mmoja’
NENO LA MUNGU.

SHANGILIO. Yohane. 6:51.
Aleluya, Aleluya! Mimi ndimi chakula chenye uzima kilichoshuka kutoka mbinguni; asema Bwana; mtu akila chakula hiki, ataishi milele.
Aleluya!

INJILI Yohane. 6:51-58.
Yesu aliwaambia Wayahudi, ‘Mimi ndimi chakula chenye uzima kilichoshuka kutoka mbinguni; mtu akila chakula hiki, ataishi milele. Na chakula nitakachotoa mimi ni mwili wangu, kwa ajili ya uzima wa ulimwengu. Basi Wayahudi walishindana wao kwa wao wakisema, “Awezaje mtu huyu kutupa sisi mwili wake ili tuule?” Basi Yesu akawaambia, ‘Amin, amin, nawaambieni, Msipoula mwili wake Mwana wa Adamu na kuinywa damu yake, hamna uzima ndani yenu. Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho. Kwa maana mwili wangu ni chakula cha kweli, na damu yangu ni kinywaji cha kweli. Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu, nami hukaa ndani yake. Kama vile Baba aliye hai alivyonituma mimi, nami ni hai kwa Baba; kadhalika naye mwenye kunila atakuwa hai kwa mimi. Hiki ndicho chakula kishukacho kutoka
mbinguni; si kama mababa walivyokula, wakafa; bali akilaye chakula hicho ataishi milele.
INJILI YA BWANA.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *